Ninamshukuru jalali, kunijalia uhai,
Na hii bora hali, shetani kwangu hakai
Bada ya hii kauli, na ninyi nawasabai
Haya ndo maendeleo, ya vijana Tanzania
Baada ya hizo salamu, sasa zafuata pongezi
Restilesi ndo muhimu, hali kuiweka wazi
N a washirika muhimu, walofanikisha kazi
Haya ndo maendeleo, ya vijana Tanzania
Katika mikoa saba, kaziyo imefanyika
Hakikuachwa kibaba, haliyo imefichuka
Tumezimaliza raba, mitaani kuzunguka
Haya ndo maendeleo, ya vijana Tanzania
Kuhusu wao uchumi, vijana wamefunguka
Bila kuminya ulimi, baadhi wachakarika
Kilimo hawakilimi, malipo si uhakika
Haya ndo maendeleo, ya vijana Tanzania
Juu ya wao uzazi, haki zao hawajui
Hawashiriki uzazi, manesi ni maadui
Mipango haiku wazi, hatima hawaijui
Haya ndo maendeleo, ya vijana Tanzania
Ushiriki mitaani, ni wachache wako mbele
Mifumo serikalini, waipigia kelele
Hawawekwi shirikani, kupewa kipaumbele
Haya ndo maendeleo, ya vijana Tanzania
Lipo hili babalao, la kuitunga katiba
Namna ushiriki wao, wanahitaji tiba
Washangaa tume yao, maoni inavyoiba
Haya ndo maendeleo, ya vijana Tanzania
Kwa uchaguzi ujao, wengi wataka shiriki
Kwa huo wao upeo, wadai ni yao haki
Mawio hata machweo, mafisadi hawataki
Haya ndo maendeleo, ya vijana Tanzania
Yapo mengi ya muhimu, ripoti itaeleza
Wapo watu wa muhimu, mwishoni nitaeleza
Keni na Fransi walimu, hadi kazi twamaliza
Haya ndo maendeleo, ya vijana Tanzania
Osca Kefa na Devidi, wao wamo miongoni
Agi Kikoti wazidi, Denisi yu ulingoni
Lau Jaco si wakaidi, Efurahimu makini
Haya ndo maendeleo, ya vijana Tanzania
Kalamu naweka chini, msifikiri frimasoni
Vijanangu komaeni, katu musione soni
Ukataeni uhuni, maendeleo usoni
Haya ndo maendeleo, ya vijana Tanzania